Licha ya kuwa na faida kubwa mwilini ulaji wa uyoga nchini bado upo chini sana; hii imetokana na kwanza, kutopatikana kwa urahisi uyoga pori kutokana na uharibifu wa mazingira; na hasa ikizingatia kuwa uyoga pori hupatikana kipindi cha masika tu. Pia bado wakulima wa uyoga ni wachache sana hivyo kupelekea walaji wengi kutegemea uyoga kutoka nje, uyoga huu kutoka nje ambao huuzwa kwenye maduka makubwa (supermarket) kwenye migahawa na mahoteli. Huwa hatuna uhakika usalama, kwa maana ya umezalishwa vipi (kutotumia kemikali zozote) na pia ubora huwa hafifu kwani hukaa muda mrefu kabla ya kutumiwa, tangu kusafirishwa na kuhifadhiwa kabla ya mlaji kuununua. Hivi sasa teknolojia ya ulimaji wa uyoga imeanza kukua kwa kasi na watanzania wengi wameanza kuzalisha hasa baada ya kuona umuhimu wake kiafya, kiuchumi na utunzaji mazingira. Hii imepelekea kupunguza changamoto ya upatikanaji wa uyoga na mlaji kuwa na uhakika na ubora.
Zifuatazo ni sababu zinazofanya watanzania kjenga mazoea ya kula uyoga na bidhaa zake mara kwa mara (walau kwa uchache mara mbili kwa wiki)
1.
Chanzo Kikubwa cha protini salama: Uyoga ni kati ya vyakula vichache sana ambavyo vinaweza kukidhi mahitaji yote ya protini mwilini. Lishe ya protini ni asilimia 20-49 kwa uyoga uliokaushwa kutegemea na aina ya uyoga. Protini inahitajiwa sana mwilini hasa kwa watoto katika kuujenga mwili, kuratibu ufanyaji kazi wa sehemu zote za mwilini, na katika kuukarabati mwili, hasa wakati wa umri unavyozidi kusonga mbele. Kundi la chakula cha protini katika nyama tulivyozoea kuila (nyama ya Ng’ombe, mbuzi, Kondoo,kuku n.k) ni asilimia 12 hadi 20 ya uzito wa nyama hiyo. Lakini nafaka nyingi tunazokula kila siku (Mahindi, Mchele, n.k), zina uhaba wa protini ; asilimia 6% hadi 9% tu. Pia protini kutoka baaddhi ya nafaka hizi, ina upungufu wa baadhi ya asidi amino (amino acids), ambazo ni kemikali maalumu zinazohitajiwa mwilini. Wanajamii wanaohangamkia ulaji wa uyoga watafurahi kufahamu kwamba Uyoga una kiwango cha juu cha protini; asilimia 19% hadi asiimia 40% kwa Uyoga mkavu. Na protini katika uyoga zina asidi amino zote muhimu kwa mwili.
2.
Chanzo cha vitamin nyingi: Uyoga una vitamini mbalimbali kama A,B,C,D,E na K; Uyoga una aina nyingi zaidi za vitamin kama vile thiamine, riboflavin, ascorbic acid, niacin, biotin, folic acid, pantothenic acid, na ergesterine. Hata hivyo Uyoga una upungufu wa vitamini A.
3. Chanzo cha madini mengi: UYOGA pia una wingi zaidi wa madini yajulikanayo kama micronutrients (kama Calcium, Phosphorus, Chuma, Zink, Magnesium, Cobalt, Shaba, Sodium, Potassium, na selenium); ambayo ni muhimu katika kujenga, kulinda afya na kudhibiti magonjwa mbalimbali mwilini. Madini mengine ni Zinki-kuimarisha kinga, Shaba (copper)-inasaidiana na Chuma kutengeneza chembechembe nyekundu za damu. UYOGA pia una wingi zaidi wa madini yajulikanayo kama micronutrients (kama Calcium, Phosphorus, Chuma, Zink, Magnesium, Cobalt, Shaba, Sodium, na selenium).
4.
Kuzuia na kutibu magonjwa mengi: kumekuwa na na mwamko mkubwa wa kufanya tafiti juu ya uyoga ; na hasa aina (species) ambazo, huko china zimekuwa zikitumiwa katika tiba kwa magonjwa mengi, tangu ya zaidi miaka 2000 iliyopita. Kwa mfano tafiti juu ya uyoga uitwao Ganoderma lucidium uitwao Schizophyllum commune na pia Trametes versicolor. Hizi pamoja na aina zingine nyingi za UYOGA zinaaminiwa kuwa na uwezo wa kupunguza makali ya magonjwa mbalimbali, au kuponya kabisa baadhi ya magonjwa, kama vile saratani (cancer), shinikizo la damu, matatizo ya moyo, figo, ngozi, vidonda visivyopona haraka n.k.
a. Tukiwa na tabia ya kula UYOGA mara kwa mara, tunajiepusha na hatari hizo kwa vile UYOGA hauna kemikali ya kolesteroli, na pia kwa vile imethibitishwa kwamba ulaji wa aina nyingi za UYOGA (kwa mfano Auricularia Auricula, Pleurotus Ostreatus na virutubishi vilivyotengenezwa kutoka kwa uyoga uitwao Ganoderma lucidum) hupunguza kolesteroli mbaya (LDL) kwenye damu.
b. Tafiti juu ya uyoga uitwao Ganoderma lucidium uitwao Schizophyllum commune na pia Trametes versicolor. Hizi pamoja na aina zingine nyingi za UYOGA zinaaminiwa kuwa na uwezo wa kupunguza makali ya magonjwa mbalimbali, au kuponya kabisa baadhi ya magonjwa, kama vile saratani (cancer), shinikizo la damu, matatizo ya moyo, figo, ngozi, vidonda visivyopona haraka n.k.
c. Aina nyingi (species) za UYOGA zina carbohydrates za kipekee (polysaccharides), ambazo mara nyingi ni glucans zenye uasili wa Glukosi , na ambazo mara nyingi zinakuwa zimeunganika kwa kwa kipekee na kemikali zingine (polypeptides), zenye asili ya protini. UYOGA tunaoula, kuumeza, na kuupitisha kwenye mfumo wetu wa chakula(elementary canal). Unatusaidia kufikisha kemikali hizi za kipekee tumboni. Utafiti wa wataalamu wengi wa sayansi unazidi kuonesha na kuthibitisha kwamba kemikali hizi za UYOGA (zenye asili ya carbohydrates zilizounganika na zingine zenye asili ya protini), zinasaidia kuupatia mwili kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na saratani za utumbo (colon cancers)
5. Kupunguza uzito: Idadi kubwa ya kemikali ndani ya UYOGA ziko katika kundi la kabohidrati (carbohydrates asilimia 50% hadi 70%). Lakini mfumo wake ni tofauti na ule wa wanga (starch) kutoka katika vyakula vya nafaka kama vile mchele, mtama au mahindi ambazo hubadilishwa na vimeng’enywa(enzymes) katika mfumo wetu wa chakula tumboni(elementary canal), na kutumiwa kama nishati ya kuuwezesha mwili kufanya kazi. Chakula ha wanga kutoka katika mimea ya nafaka au viazi n.k kikizidi mwilini, hubadilishwa na kuwa mafuta. Ongezeko la mafuta haya katika mwili ndio chanzo cha mtu kuzidi kunenepa na kuwa ana kitambi. Lakini kabohidrati za asili ya UYOGA kutokana na mfumo wake wa kipekee, haziwezi kushughulikiwa na kubadilishwa na vimeng’enya katika mfumo wetu wa chakula. Kwa hiyo hubaki kama dietary fibres, ambazo hazimletei mlaji tatizo la mafuta mengi, unene usio wa kawaida, au kitambi cha kumletea shida. Kwa sababu hiyo tunaweza kuzibatiza dietary fibres za UYOGA, kuzipatia jina la sliming agents.
6. Usalama
Kiafya: Kilimo cha uyoga kinafuata
kanuni za kilimo hai; ni salama kiafya kwani hakitumii viwatirifu na viuadudu;
na huhutaji mazingira safi na usafi wa hali ya juu ili kuweza kuuzalisha.
7. Ladha tamu: Uyoga ni moja ya chakula chenye ladha tamu mdomoni hasa ukipikwa vizuri;
hivyo humfurahisha mlaji. Walaji wengi
hukiri kuwa ladha ya Uyoga ni tamu kuliko ladha ya nyama.
8.Mapishi mbalimbali na bidhaa mbalimbali Jamii mbalimbali zimeweza kubuni mapishi mengi kwa
kutumia uyoga. Baadhi tu ya mapishi ambayo uyoga unaweza kupikwa ni kama;Supu
ya Uyoga, Kitoweo cha Uyoga. Vitafunwa; sambusa, keki n.k, Piza ya Uyoga, Uyoga
kuchangaywa(Kutumika kama kiungo) na vyakula vingine kama nyama, samaki, mboga
za majani. Mishikaki ya Uyoga/Uyoga wa kuchomwa, Makange ya Uyoga. Pia uyoga
unaweza kutengenezewa bidhaa mbalimbali biskuti, shampeni, juisi, mvinyo,
achali n.k
9.Utunzaji wa mazingira: Kilimo cha uyoga hutumia masalia ya mazao mbali mbali kama majani ya mgomba, ngano na mpunga, maranda, vumbi la mbao, maganda ya karanga, alizeti n.k. ambayo yakiachwa kwenye mazingira huleta uharibifu mkubwa. Pia baada ya kuvuna vimeng’enywa (udongo ulitumiwa kuoteshea uyoga) hutumika kama chakula cha wanyama, mbolea na kuzalisha nishati kama biogas, mkaa n.k. Hivyo ulaji wa Uyoga mara kwa mara mlaji anashiriki katika a kupunguza uchafuzi wa mazingira.
10. Kuinua uchumi: Kilimo cha uyoga ni chanzo mojawapo cha kuongeza Kipato kwa wanachi hivyo kuinua kiwango cha ajira na uboreshaji uchumi. Ulaji uyoga kwa wingi utachochoea uzalishaji Uyoga kwa wingi hivyo kuinua pato la mkulima, na kuinua uchumi, kuchangia upatikanaji na usalama wa chakula, kuinua kiwango cha lishe, kupunguza njaa na kiwango cha umaskini nchini. Pia badala ya kuwa waagizaji wakubwa wa Uyoga, Tanzania itaweza kuuza uyoga nje ya nchi kama zao la biashara na kujipatia fedha za kigeni.
Kwa maelezo zaidi, ushauri, upatikanaji, mapishi na mafunzo ya kilimo cha uyoga.